WATU 479 wameuawa nchini kutokana na vitendo vya ukatili ukiwamo wa watu kujichukulia sheria mkononi katika kipindi cha nusu mwaka 2017, ikiwa ni mara tatu ikilinganishwa na mwaka uliopita, jambo linaloonesha kuwapo ukiukwaji wa haki.
Aidha katika matukio hayo, Mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa watu kujichukulia sheria mkononi kwa kuwa na matukio 117 yaliripotiwa polisi, ukifuatiwa na Mkoa wa Mbeya wenye matukio 33, Mara (28) na Geita (26).
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Helen Kijo Bisimba amebainisha hayo jana jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa ripoti ya hali ya haki za binadamu kwa kipindi cha nusu ya Mwaka 2017.
Ripoti hiyo inaonesha hali za binadamu kuwa bado ni mbaya kwa kipindi cha nusu mwaka ikilinganishwa na miaka iliyopita ambapo Dk Bisimba amesema ripoti hiyo inayoanzia Januari hadi Juni mwaka huu ,inaonesha kuwepo kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za kiraia hususani haki ya kuishi, lakini pia ukiukwaji mkubwa wa haki za makundi maalumu wakiwemo wanawake na watoto.
Amesema Jeshi la Polisi linapaswa kushughulikia haraka tatizo la kuwapo matukio hayo na kuhakikisha watuhumiwa wa matukio hayo wanafikishwa mbele ya sheria.
