Watu wasiopungua 12 wameuawa jana katika shambulio la kujitoa muhanga na risasi dhidi ya mgahawa maarufu katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu.
Afisa wa polisi Ali Hassan amesema mripuaji wa kujitoa muhanga alijiripua kwenye gari katika lango la mgahawa wa Bosh Treats, ambao pia unahudumu kama hoteli, na kuuwa walinzi na raia.
Mripuko huo pia ulishambulia kwa sehemu mgahawa wa jirani.
Maafisa usalama wanaamini washambuliaji wenye silaha pia walijigawa katika makundi mawili, na kuvamia migahawa yote, na kuchukuwa watu mateka katika jengo la pili. Kundi la Al-Shabaab limedai kuhusika na shambulizi hilo kupitia kituo chake cha redio cha Andalus.
Watu kadhaa waliokolewa katika mgahawa wa kwanza, kwa mujibu wa afisa usalama wa Somalia Mohammed Hassan.
Miongoni mwao walikuwemo wageni kutoka Kenya na Somalia waliokuwa wanafanyakazi katika mgahawa huo.
