Watu wawili wameuwawa na wengine wanne wamejeruhiwa vibaya hapo jana katika ghasia za nchini Venezuela wakati upinzani wa kisiasa ulipoitisha kura ya maoni isiyo rasmi ya kupinga mipango ya Rais Nikolas Maduro ya kuiandika tena katiba ya nchi.
Kulingana na msemaji mkuu wa upinzani, watu wenye silaha waliokuwa wamepanda pikipiki walikishambulia kituo cha kupigia kura katika mji wa Catia, kaskazini magharibi mwa mji mkuu wa Caracas.
Taifa hilo lenye utajiri wa mafuta linakabiliwa na mgogoro mbaya wa kiuchumi kuwahi kutokea, huku kukiwa na uhaba wa mahitaji kadhaa ya msingi pamoja na mfumko wa bei wa hali ya juu.
Zaidi ya watu 90 wameuwawa katika maandamano ya kila siku ya kuipinga serikali iliyopo madarakani yaliyoanza tokea mwezi Aprili mwaka huu.
Maduro ambaye amekataa kuachia madaraka, pia ameitisha kura ya maoni baadaye mwezi huu ya kuteua kamati maalumu itakayoandika upya katiba ya taifa hilo la Amerika Kusini.
