SERIKALI imewaonya watumishi wa umma waliotajwa kuhusika na kughushi vyeti wapatao 9,932 kwamba wasifanye mzaha na suala hilo na kwamba wanaokusudia kukata rufaa, ikibainika wameendelea kuidanganya serikali, watapata adhabu kubwa zaidi.
Aidha, imebainika kwamba wapo watu wanaopata mamilioni kwa kuwahadaa, walioingia kwenye orodha ya watumishi wenye vyeti feki kwa kutoa kati ya Sh milioni moja hadi Sh milioni nne, ili kuondolewa katika orodha hiyo.
Kwa nyakati tofauti mjini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Laurean Ndumbaro, wametoa kauli za kuonya kuhusu watumishi hao wenye vyeti feki kuwa wasifanye mzaha na suala hilo.
Akijibu mwongozo bungeni jana, Kairuki amesema wote wenye malalamiko halali, waandike barua kwa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kupitia kwa waajiri wao kulalamika.
Amesema wanaolalamika kuwa wameonewa huku wanajua kwa uhakika kwamba walighushi vyeti vyao, ikibainika wameendelea kuidanganya serikali watapata adhabu kubwa.
Kairuki amesema taarifa ya uhakiki ilivyotoka Aprili 28, mwaka huu wapo ambao wamekubali na kuachia ofisi kabla ya Mei 15, mwaka huu ambayo ni siku ya mwisho na wengine wanapinga kwamba hawana vyeti feki.
Mapema bungeni, Mbunge wa Viti Maalumu, Conchesta Rwamlaza (CCM) aliomba mwongozo akisema baadhi ya watu wamelazwa hospitalini kutokana na kutajwa kwenye orodha ya watu wenye vyeti feki.
Dk Ndumbaro amesema vyeti hivyo wanaangalia index namba na gamba la vyeti vyenyewe, nakala hizo za vyeti vilivyoskaniwa au nakala laini, zinaweza kutumwa kwa njia ya barua pepe ya Necta na wizara kabla ya Mei 15, mwaka huu.
