Waziri Mkuu awahakikishia wawekezaji,Tanzania ni nchi yenye amani, utulivu wa kisiasa na uchumi

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewahakikishia uwekezaji wenye tija wawekezaji watakaokuja nchini kwa kuwa Tanzania ni nchi yenye amani, utulivu wa kisiasa na uchumi wenye kukua kwa kasi.

Ameyasema hayo jijini Dar es Salam alipomuwakilisha Rais John Magufuli katika maadhimisho ya miaka 60 tangu Mtukufu Aga Khan ,alipochaguliwa kuwa Imamu Mkuu wa madhehebu ya Shia Ismailia duniani.

Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua na kuthamini shughuli mbalimbali zinazofanywa, na mtandao wa taasisi za Aga Khan zilizopo hapa nchini, hivyo Serikali itaendelea kushirikiana nao.

Aliupongeza mtandao wa taasisi za Aga Khan kwa kumuunga mkono Dk Magufuli katika kutoa kipaumbele cha kuwapa fursa watu wenye kipato cha chini kushiriki katika uzalishaji ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Kwa upande wake Rais wa Jumuiya ya Madhehebu ya Shia Ismailia Tanzania, Amin Lakhani ameishukuru Serikali kwa ushirikiano inaowapa na kwamba ameahidi kuendelea kushirikiana nayo katika kuboresha sekta mbalimbali nchini.

Amesema mtandao wa maendeleo wa Aga Khan unatoa huduma mbalimbali zikiwemo za afya, elimu, kilimo na kunaendesha miradi katika mabara ya Afrika na Asia kwa kuwapa fursa watu wenye kipato cha chini kushiriki katika uzalishaji ili kujikwamua kiuchumi.

 

Exit mobile version