Waziri Mkuu awaomba viongozi wa dini kuwahimiza wazazi na walezi kuishi maisha yenye nidhamu

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amewaomba viongozi wa dini nchini kutumia nafasi zao kuhimiza wazazi na walezi kuishi maisha yenye nidhamu, kuthamini kazi yenye kumpendeza Mwenyezi Mungu na kusimamia malezi ya watoto na kuzingatia maadili ya Taifa kwa ujumla.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo, wakati akifungua kongamano kuhusu mmomonyoko wa maadili na athari za dawa za kulevya lililoandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, lililofanyika mjini Dar es Salaam.

Amesema kila mzazi au mlezi aone aibu, uchungu na ajutie anapoona mtoto yoyote akienda kinyume na utaratibu wa kawaida wa maisha na ni vema wakatumia nafasi yao kwa kuwahimiza vijana hao waishi maisha ya nidhamu na yenye kumpendeza Mwenyezi Mungu.

Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kujenga jamii yenye kuzingatia maadili nchini na Mheshimiwa Rais, Dkt. John Magufuli amekuwa akiwasisitizia Watanzania wote kuzingatia maadili katika jamii kwa kufanya kazi kwa bidii na kujiepusha na vitendo vyote vya rushwa na ubadhirifu.

 

Exit mobile version