Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amekutana na mabalozi wa Tanzania wanaokwenda kuiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali na kuwataka kuhakikisha wanaimarisha uhusiano na kujenga urafiki na nchi wanazowakilisha, kwa lengo la kuitangaza Tanzania kiuchumi ikiwa ni pamoja na kueleza fursa za uwekezaji zilizopo nchini.
Waziri Mkuu amewaeleza mabalozi hao kuwa Tanzania inazo fursa nyingi za uwekezaji na jukumu lao la kwanza ,ni kuzitangaza ili kuleta wawekezaji wengi nchini.
Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano imelipa kipaumbele suala la ushirikishwaji sekta binafsi.
Akizungumzia suala la Watanzania waishio nje ya nchi, amewataka mabalozi kuwakutanisha na kufanya nao mikutano mara kwa mara ,ili kujua kama wana matatizo yanayoyapata katika nchi wanazoishi, ili kuangalia jinsi kuweza kusaidiwa.
Mabalozi wa Tanzania walioteuliwa hivi karibuni na Rais John Magufuli nje ya nchi, walifika Ofisi ya Waziri Mkuu mjini Dodoma mwishoni mwa wiki kwa lengo la kumuaga na kwenda kuanza majukumu yao katika nchi walizopangiwa.
Mabalozi hao wanakwenda kuiwakilisha Tanzania katika nchi za Qatar, Ubelgiji, Afrika Kusini, Ujerumani, Comoro, Algeria, India na Sudan.
