Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema ili taifa liweze kuwa na watu waadilifu na wachapakazi, ni muhimu kwa wazazi kuhakikisha wanalifanyia kazi jukumu la kulea watoto kwenye misingi ya kumcha Mungu na muda mwingine kuhoji watoto kuhusu utajiri wanaoupata ghafla.

Majaliwa amesema kuwa Taifa la watu waadilifu na wachapakazi huanzia katika ngazi ya familia,  na  Kama kaya  haziishi kwa uadilifu, ni vigumu sana kuwa na taifa lenye wananchi waadilifu.
Waziri Mkuu ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na wageni ,waliohudhuria harambee ya kuchangia ujenzi wa kanisa na nyumba ya Paroko katika Parokia teule ya Zuzu, nje kidogo ya mji wa Dodoma.
Harambee hiyo ilitanguliwa na ibada ya misa ya shukrani kwa ajili ya marehemu Mzee Xavery Mizengo Pinda, ambaye ni baba yake, Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda.
Mzee Xavery Pinda alifariki Novemba 27, mwaka jana katika hospitali ya mkoa wa Dodoma na kuzikwa kijijini kwake Kibaoni wilayani Mlele, Katavi.
Katika harambee hiyo, Waziri Mkuu na mke wake walichangia Sh milioni 10 ambapo jumla ya Sh milioni 160 zilikusanywa.
Kati ya hizo, Sh milioni 111.15 zilikuwa ni ahadi, Sh milioni 38.45 zilikuwa ni fedha taslimu na Sh milioni 10.403 zilikuwa ni thamani ya vifaa vya ujenzi vilivyotolewa.
Exit mobile version