Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe wiki hii atazuru Urusi ambako atakuwa na mazungumzo na Rais Vladimir Putin mnamo wakati nchi hizo mbili zikijaribu kutafuta suluhisho la mzozo wa mipaka uliodumua kwa miaka mingi.
Ikulu ya Urusi, Kremlin, imesema hii leo kuwa mazungumzo ya viongozi hao yataangazia ushirikiano kati ya nchi hizo katika nyanja za kisiasa, biashara, uchumi na masuala ya kibinadamu.
Ziara hiyo inafuatia ziara ya Rais Putin nchini Japan mwezi Desemba mwaka jana ambayo ni ya kwanza katika kipindi cha miaka 11.
Hata hivyo, kwenye ziara hiyo ya Desemba, Putin na Abe walishindwa kupata ufumbuzi wa mzozo juu ya visiwa kadhaa, ambao umeyafanya mataifa hayo mawili hadi sasa kushindwa kusaini makubaliano rasmi ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia.
Siku hizo ikiitwa Jamhuri ya Muungano wa Kisovieti, Urusi ilivichukuwa visiwa kadhaa kaskazini mwa pwani ya Japan, mnamo mwaka 1945, wakati Vita hivyo vikikaribia ukingoni.
Tangu hapo, visiwa hivyo vimekuwa kiini cha mzozo mkubwa kati ya Urusi na Japan.
