Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May amewasili nchini Japan kwa ziara rasmi, akilenga kutuliza wasiwasi kuhusu hatua ya Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya na kuanzisha mazungumzo ya mapema kuhusu biashara huria na taifa hilo la tatu kiuchumi duniani.
May anatarajiwa kukutana na mwenyekiti wa kampuni ya kutengeneza magari ya Toyota wakati wa ziara yake hiyo ya siku tatu ambayo inaanzia mjini Osaka kabla ya kuelekea Tokyo ambako atakutana na Mfalme Akihito na Waziri Mkuu Shinzo Abe.
Hatua ya Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya ilizusha wasiwasi nchini Japan kuhusu athari za hatua hiyo kwa kampuni zenye maslahi makubwa ya kibiashara nchini humo.
Afisa wa wizara ya Mambo ya Kigeni ya Japan anayehusika na masuala ya Umoja wa Ulaya alisema kabla ya ziara ya May kuwa watataka uwazi na uhakika kutoka kwa Uingereza ili kupunguza athari zinazoweza kutokea kwa kampuni za Japan.
