Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Sigmar Gabriel, amefanya ziara ya ghafla nchini Somalia, ambako ameahidi kuongeza mara mbili msaada wa nchi yake kwa taifa hilo lililoathiriwa vibaya, na ukame katika Pembe ya Afrika.
Gabriel amewasili mjini Mogadishu jana kukiwa na ulinzi mkali, na hiyo ikiwa ziara ya kwanza ya waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani nchini Somalia.
Waziri huyo ameonya kuwa miaka kadhaa ya ukame inasababisha janga la kibinaadamu ,ambalo linahitaji msaada mkubwa kutoka nje.
Tayari, Ujerumani ilikuwa imeshaahidi msaada wa dola milioni 76 kwa Somalia, ambako zaidi ya watu milioni sita wanauhitaji mkubwa wa msaada wa kiutu.
Katika mkutano wake na Waziri Mkuu wa Somalia, Hassan Ali Khaire, Sigmar Gabriel amesema Ujerumani iko tayari kuongeza maradufu msaada huo.
