Baadhi ya Wenyeviti wa Chama cha Wafugaji nchini (CCWT) ambao wanatoka katika Kanda saba za kifugaji nchini,wanatarajia kwenda kwa Msajili wa Wizara ya Mambo ya ndani ya nchi wa vyama vya ushirika, kwa lengo la kushinikiza uchaguzi wa viongozi ufanyike katika Chama chao.
Hatua ya Wenyeviti hao kwenda kwa Msajili huyo wa Vyama inatokana na wao kutokuwa na imani na uongozi wa sasa ambao ni wa mpito, na wanadai kuwa umekuwa ukikiendesha Chama hicho kidiktekta licha ya muda wao wa kuwa madarakani kwisha.
Kauli hiyo imetolewa leo Mjini Dodoma na Wenyeviti hao wakati wakizungumza na waandishi wa habari baada ya kutofautiana katika mkutano mkuu wa wafugaji.
Mmoja wa Wenyeviti hao,WAMARWA KUSUNDA amesema kuwa waliuchagua uongozi wa mpito ambao ni mwenyekiti,katibu mkuu,mtunza hazina pamoja na wajumbe 12 wa kamati tendaji mnamo mwaka 2015 kwa lengo la kutetea maslahi ya wafugaji.
Hata hivyo amesema kuwa Serikali kupitia Mkamu wa Rais Samia Suluhu Hassan aliwaagiza Wakuu wa wilaya nchini, kwa kushirikiana na viongozi wa wafugaji kutenga maeneo ya malisho lakini suala hilo halijatekelezwa na badala yake Uongozi huo, unataka kwenda kwa makamu wa rais kulalamikia kuwa maeneo hayajatengwa jambo ambalo ni kutaka kuwachonganisha na wakuu hao wa wilaya.
