WIZARA ya Nishati na Madini imesisitiza kuwa itaendelea kutumia watalaamu, kupata ushauri wa maeneo yanayohitaji kufanyiwa utafiti wa mafuta na gesi ,na haitaliacha suala hilo liingiliwe kisiasa.
Msimamo huo umetolewa bungeni Dodoma jana na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo wakati akijibu swali la nyongeza la mbunge wa viti maalum, Susan Lyimo (Chadema).
Lyimo ametaka kujua ni kwanini serikali haimtumii mzee maarufu katika mji wa Mlimba, anayedaiwa kuwa na taarifa kamili kuhusu uwepo wa mafuta kwenye bwawa lililopo mjini hapo, ili lifanyiwe utafiti.
Akijibu maswali hayo, Profesa Muhongo amesema serikali haiwezi kwenda kwa mzee yeyote kuuliza taarifa za utafiti wa mafuta na gesi ,kwa kuwa suala hilo ni la kitaaluma zaidi na utafiti wake hufanyika baada ya wataalam kuwa na uhakika, wa uwezekano wa kupatikana kwa nishati hizo
Aidha amesema katika utafutaji wa mafuta duniani, wakati mwingine utafiti huonesha kuwepo au ukosefu wa nishati hiyo, na kwa sasa Tanzania ina mpango wa kubadilisha mbinu ya utafutaji wa mafuta hayo.
