Zaidi ya watu 14 wameuawa nchini Somalia baada ya makabiliano kuzuka kati ya wanajeshi na raia kuhusiana na msaada wa chakula.
Maafisa wanasema wengi wa waliokufa ni raia ambao walijikuta katikati ya vurugu hizo kati ya makundi mawili ya wanajeshi, ambapo baadhi yao walijaribu kuiba magunia ya chakula kilichostahili kupewa watu waliopoteza makaazi.
Makabiliano hayo yalitokea katika mji wa kusini magharibi wa Baidoa, ambao umeshuhudia mmiminiko wa maelfu ya watu kufuatia hali mbaya zaidi ya ukame kuwahi kutokea katika zaidi ya miaka 70.
Somalia ni moja kati ya nchi nne zilizochaguliwa na Umoja wa Mataifa katika mpango wa ombi la msaada wa dola bilioni 4.4 ili kuepusha janga la njaa pamoja na Nigeria, Sudan Kusini na Yemen
