Zimbabwe itajenga chuo kwa gharama ya dola bilioni moja, kwa hemisha ya mtu anayelaumiwa kwa kuiongoza nchi kuelekea hali ngumu ya uchumi, Robert Mugabe.
Jonathan Moyo, ambaye ni waziri wa elimu aliwaambia waandishi wa habari kuwa wanachukua hatua hiyo kwa heshima ya rais huyo wa umri wa miaka 93, kwa wajibu wake katika elimu na uongozi mzuri.
Haijulikani pesa hizo zitatoka wapi kwenye nchi ambayo ukosefu wa ajira na umaskini ni tatizo kubwa.
Mwaka uliopita zaidi ya watu watu milioni moja nchini Zimbabwe walikumbwa na ukosefu wa chakula kotokana na ukame. Nchi hiyo wakati mmoja ilitajwa kuwa ghala la Afrika.
Licha ya hilo baraza la mawaziri limekubali kutumia dola milioni 800 kujenga chuo hicho kipya huko Mazowe, kilomita 35 nje ya mji wa Harare.
