Mwili wa kiongozi wa zamani wa upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Etienne Tshisekedi umewasili kwenye mji mkuu wa nchi hiyo Kishasa kutoka Ubelgiji ikiwa ni miaka miwili tokea kufariki kwake. Tshisekedi aliyefariki akiwa na umri wa miaka 84 alikuwa kiongozi wa upinzani kwa miongo kadhaa nchini Kongo, kabla ya kifo chake mwaka 2017 nchini Ubelgiji. Kurejeshwa kwa mwili wake kunatimiza mojawapo ya ahadi za mwanawe Felix Tshisekedi ambaye aliingia madarakani kama rais Kongo mapema mwaka huu. Maelfu ya watu wanatarajiwa leo kuhudhuria ibada ya kuuaga mwili wa Tshisekedi katika uwanja wa mpira mjini Kinshasa. Viongozi wa mataifa sita ya Afrika wanatarajiwa kuhudhuria mazishi yatakayofanyika kesho Jumamosi.