Mahakama ya Kijeshi nchini Kongo (DRC) imemhukumu kifo Rais wa zamani Joseph Kabila kwa kukosa kuhudhuria kesi yake (in absentia), baada ya kupatikana na hatia ya uhalifu wa kivita, uhaini na uhalifu dhidi ya binadamu.
Kesi hiyo inahusishwa na madai ya usaidizi wake kwa waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda mashariki mwa DRC. Jaji Mkuu wa Kijeshi, Luteni Jenerali Joseph Mutombo Katalayi, alisema Kabila ametiwa hatiani kwa makosa ya mauaji, ubakaji, mateso na uasi.
Kabila, aliyeongoza taifa kuanzia 2001 hadi 2019, amekanusha tuhuma na kudai mchakato wa kisheria umeingiliwa kisiasa. Mahakama pia imemwamuru kulipa fidia ya takribani dola bilioni 50 kwa serikali na waathiriwa.
Tuhuma dhidi ya Kabila zimeibua hofu ya kuongeza mgawanyiko nchini humo, hasa kutokana na mapigano ya muda mrefu mashariki mwa DRC ambapo waasi wa M23 sasa wanadhibiti maeneo makubwa ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.
Serikali ya Rais Félix Tshisekedi tayari imesitisha chama cha kisiasa cha Kabila na kuchukua mali za viongozi wake, huku Rwanda ikiendelea kukanusha kuhusika moja kwa moja katika vita hivyo.
#radio5fm



