Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ameagiza miradi yote yenye thamani ya ujenzi isiyozidi bilioni 10 ,wapewe Wakandarasi wa ndani ili kukuza pato la taifa.
Akifungua mkutano wa mashauriano wa Bodi ya usajili wa makandarasi wa mwaka 2017,mjini Dodoma Amesema kuwa wakandarasi hao wapewe miradi hiyo, ili waweze kuzalisha ajira kwa vijana wengi wa kitanzania waliopo mtaani.
Aidha samia amesema kuwa Serikali itaendelea kuwapa kipaumbele wakandarasi wazawa ,ili wamudu zabuni za ujenzi kwani kwa kufanya hivyo kutaleta faida mbalimbali ikiwemo fedha watakazopata, kwani wataweza kuwekeza ndani ya nchi na kutoa ajira.
Naye Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amesema kuwa kuwa Wizara hiyo inaendelea kusimamia sheria na maadili kwa wakandarasi ili kuhakikisha miradi ya ujenzi inayotekelezwa kote inakuwa na ubora unaotakiwa.
Kwa upande wake, Msajili wa Bodi ya Wakandarasi Nchini, Rhoben Nkori amesema bodi hiyo imefuta usajili wa wakandarasi 3,000 kwa kushindwa kutimiza matakwa ya Usajili wa Wakandarasi ya mwaka 1997 na kwa sasa bodi hiyo inawakandarasi 9,000 kote nchini.
