Wizara ya usafiri ya Misri imesaini makubaliano na kampuni za China katika kujenga reli nyepesi ya kasi yenye thamani ya dola bilioni 1.24 za kimarekani katika maeneo mapya mjini Cairo.
Reli hiyo mpya yenye urefu wa kilomita 66 na vituo 11, itaunganisha mji mkuu mpya wa utawala unaoendelea kujengwa na maeneo ya Cairo Kuu.
Waziri mkuu wa Misri Bw Sherif Ismail, waziri wa usafiri Bw Hesham Arafat pamoja na balozi wa China nchini Misri Bw Song Aiguo wamehudhuria hafla ya kusaini makubaliano kati ya Shirika la Usafiri la Misri NAT na kampuni ya usafiri wa anga ya China AVIC INTL na kampuni ya reli ya China.
Mkurugenzi wa shirika la usafirishaji la Misiri NAT amesema mradi wa reli hiyo utaanza ndani ya miezi miwili au mitatu, na inatarajiwa kusafirisha abiria laki 3.4 kwa siku.
Kampuni ya China, imesema ujenzi wa reli hiyo utatoa nafasi nyingi za ajira kwa Wamisri.
