Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amezindua shule ya awali na msingi ya mchepuo wa Kiingereza ya Chief Zulu Songea mkoani Ruvuma siku ya Jumanne Septemba 24, 2024 ambapo alikata utepe katika jengo la utawala la shule hiyo kuashiria rasmi uzinduzi huo.
Kuzinduliwa kwa shule hii, kunaonesha kusonga kwa safari ya maendeleo ya elimu nchini Tanzania hasa kwa watoto kwa kutoa fursa kwao kujifunza lugha ya kimataifa, kukuza uelewa wa tamaduni mbalimbali, na kuwasaidia watoto kuwa na ufanisi katika maisha yao ya baadaye.
Awali akizungumza kwa ufupi katika uzinduzi wa shule hiyo waziri wa tawala za mikoa na serikali za mitaa Mohamed mchengerwa amesema kuwa hayo ni mapinduzi ya elimu hapa nchini na imegharimu Zaidi ya million mia sita.
Katika hotuba yake wakati akizindua shule hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa wito wa kuangalia umuhimu wa lugha za kimataifa katika mfumo wa elimu nchini, ili kuwasaidia watoto kujiandaa
vyema kwa soko la ajira la kimataifa na kuwa mabalozi wa Tanzania katika sekta mbalimbali za kiuchumi.
Aidha Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan,amesema hakuna mwananchi atakayeguswa na mradi unaotekelezwa na Serikali asilipwe fidia Ingawa inaweza kuchelewa, ila amesema Serikali itahakikisha inampa kila mwananchi haki yake anayostahili.
Rais Samia amesema hayo leo Jumanne, Septemba 24, 2024 alipozungumza na wananchi wa Madaba mkoani Ruvuma, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya siku sita mkoani humo aliyoianza jana Jumatatu.



