Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amehudhuria kongamano la kitaifa la viwanda lililofanyika katika Ukumbi wa Kichangani mjini Iringa ambapo amesema nia ya serikali ya kuanzisha viwanda ni kutengeneza ajira kwa Watanzania.
Waziri Mwijage amesema hayo wakati wa maandalizi ya kuelekea kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Dunia, ambayo kitaifa yanatarajiwa kufanyika mkoani Iringa.
Mwijage amesema, Serikali imedhamiria kuongeza ajira kupitia sekta ya viwanda lakini pia uwepo wa viwanda umekuwa ukiongeza thamani ya mazao sehemu husika.
Amezitaka Serikali za mikoa na wilaya ziendelee kutenga maeneo kwa ajili ya viwanda.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana, Wazee na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama ameviasa viwanda nchini kufuata sheria za kazi kwa kuhakikisha usalama mahala pa kazi.