Mgomo mkubwa kabisa wa usafiri wa treni unaanza hii leo
nchini Uingereza.
Zaidi ya wafanyakazi 50,000 wa reli watagoma hii leo,
Alhamisi na Jumamosi wakishinikiza kuboreshewa malipo,
mazingira na kulalamikia kupunguzwa nafasi za ajira.
Katibu mkuu wa chama cha wafanyakazi wa reli na usafirishaji
wa majini, RMT, Mick Lynch amesema hawana namna zaidi ya
kuwatetea wanachama wao na kumaliza mvutano, ingawa
mazungumzo ya dakika za mwisho hayakuzaa matunda,
ikimaanisha mgomo huo utaendelea.
Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson amesema vyama vya
wafanyakazi havisaidii bali vinawaumiza watu wanaodai
wanawasaidia. Vyama hivyo vimeonya mgomo huo unaweza
kuchochea sekta nyingine kufuata mkondo huo.



