Wizara ya Katiba na Sheria Ikiongozwa na Waziri Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, Ofisi ya Wanasheria wa Tanganyika TLS chini ya Rais wake Wakili Boniface Mwabukusi na wakuu wa Taasisi na idara mbalimbali za serikali,Machi 28, 2025, wanatarajiwa kuwa sehemu ya uzinduzi wa Siku kumi za msaada wa kisheria kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha.
Kulingana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda, Msaada huo wa kisheria umefadhiliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, ikiwa ni matokeo ya Msaada wa kisheria wa Mama Samia uliofanyika Machi 1-7, 2025 ambapo kujitokeza kwa idadi kubwa ya wananchi kumemfanya Rais Samia kutuma tena wanasheria ili kuwasikiliza na kuhudumia wananchi ambao hawakupata fursa hiyo hapo awali.
Mhe. Makonda katika maelezo yake ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye uzinduzi wa msaada huo wa kisheria Ijumaa Machi 28, 2025 kwenye viwanja vya Ngarenaro ambapo huduma na elimu za kisheria zitatolewa, utoaji wa huduma za Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Polisi pamoja na idara na ofisi mbalimbali za serikali ambazo zitatoa huduma za bure kwa wananchi.
Wakati akihutubia kwenye maadhimisho ya miaka minne ya Rais Samia Madarakani Jana Machi 24, 2025, Mhe. Makonda amesema Mara baada ya uzinduzi huo, Wanasheria hao watagawanywa kwenye Wilaya zote za Mkoa wa Arusha chini ya Ofisi za wakuu wa Wilaya, akihimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye uzinduzi huo kama sehemu ya shukrani pia kwa Rais Samia kwa kuwaletea na kufadhili msaada huo wa kisheria.
