Arsenal Hatimaye Watwaa Taji la Premier League Baada ya Miaka 22 ya KusubiriNa Semio Sonyo – Radio 5

In Kimataifa, Michezo, Uncategorized

Klabu ya Arsenal hatimaye imeandika historia mpya kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England (Premier League) baada ya kusubiri kwa zaidi ya miaka 22, kufuatia ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Crystal Palace katika mchezo wa mwisho wa msimu uliochezwa katika Uwanja wa Selhurst Park siku ya Jumapili.

Shangwe kubwa zilitawala ndani na nje ya dimba hilo huku mashabiki wa Arsenal wakishuhudia timu yao ikiinua rasmi taji la ligi kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2004. Baada ya presha ya ushindani wa muda mrefu, hatimaye kikosi cha kocha Mikel Arteta kilitimiza ndoto ya kurejesha ubingwa wa England Kaskazini mwa London.

Sherehe za ubingwa zilianza mapema baada ya Manchester City kupoteza dhidi ya Aston Villa, matokeo yaliyothibitisha rasmi Arsenal kuwa mabingwa wa Premier League msimu wa 2025/26. Mashabiki wa Arsenal walifanya shangwe kubwa katika maeneo mbalimbali ya London kabla ya timu hiyo kukusanyika Selhurst Park kwa ajili ya mchezo wa mwisho wa msimu na hafla ya kuinua kombe.

Ingawa Arsenal waliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Crystal Palace, wengi wa mashabiki hawataikumbuka mechi hiyo kwa matokeo yake, bali kwa tukio la kihistoria la kuinuliwa kwa kombe hilo. Baada ya Palace kumaliza hafla yao ya mwisho wa msimu na kuwashukuru mashabiki wao, jukwaa liliachiwa Arsenal kuanza shamrashamra zao rasmi za ubingwa.

Wafanyakazi wa Arsenal waliingia uwanjani wakiwa wamevalia jezi nyeupe za ugenini huku wachezaji wakifuata wakiwa katika jezi nyekundu za kawaida za klabu hiyo. Mgongoni mwa kocha Mikel Arteta na kikosi chake kulikuwa na maandishi “Champions 26” kuashiria ubingwa wa mwaka 2026.

Kila mchezaji aliitwa mmoja mmoja kupokea medali yake kabla ya nahodha Martin Ødegaard kupewa heshima ya kulinyanyua kombe hilo mbele ya maelfu ya mashabiki waliokuwa wakishangilia kwa nguvu. Wachezaji nyota Declan Rice na Bukayo Saka walionekana wakilibusu kombe hilo kabla ya kuinuliwa rasmi.

Fataki nyekundu, vipande vya karatasi vilivyorushwa hewani pamoja na nyimbo za mashabiki vilitawala anga la Selhurst Park katika tukio ambalo sasa limeingia rasmi katika historia ya Arsenal. Kocha Mikel Arteta alionekana akizunguka uwanjani akiwa amelibeba kombe hilo huku akishangiliwa na mashabiki pamoja na wachezaji wake.

\

Mafanikio hayo yanatajwa kuwa matokeo ya mabadiliko makubwa yaliyofanywa ndani ya klabu hiyo katika miaka ya hivi karibuni. Wamiliki wa klabu hiyo, Kroenke Sports Enterprises, ambao zamani walikuwa wakikumbwa na upinzani mkubwa kutoka kwa mashabiki, sasa walipokelewa kwa shangwe kutokana na uwekezaji walioufanya katika kikosi na benchi la ufundi.

Safari ya Arsenal kuelekea ubingwa imekuwa ya changamoto kubwa. Mwaka 2017, klabu hiyo ilipoteza kwa mabao 3-0 dhidi ya Crystal Palace katika uwanja huohuo wa Selhurst Park, hali iliyowafanya mashabiki wengi kumtaka aliyekuwa kocha Arsène Wenger kuondoka. Miaka kadhaa baadaye, Mikel Arteta naye aliwahi kuomba radhi kwa mashabiki baada ya kipigo kingine katika uwanja huo.

\

Hata hivyo, msimu huu umeonyesha sura tofauti kabisa ya Arsenal. Timu hiyo imeonyesha uthabiti mkubwa, nidhamu ya hali ya juu pamoja na uwezo mkubwa wa kushindana hadi dakika za mwisho za msimu.

Katika mchezo huo wa mwisho, Arteta alifanya mabadiliko makubwa kwenye kikosi chake huku baadhi ya nyota wakipewa mapumziko kutokana na maandalizi ya fainali ya UEFA Champions League dhidi ya Paris Saint-Germain. Crystal Palace pia walifanya mabadiliko wakijiandaa kwa fainali ya UEFA Conference League dhidi ya Rayo Vallecano.

Kipa Kepa Arrizabalaga alipata nafasi ya kucheza mechi yake ya kwanza ya Premier League akiwa golini kwa Arsenal huku Christian Norgaard akianza kwa mara ya kwanza kwenye ligi. Max Dowman aliandika historia kwa kuwa mmoja wa wachezaji wenye umri mdogo zaidi kuanza mchezo wa Premier League akiwa na miaka 16 na siku 144.

Bao la kwanza la Arsenal lilitokana na shambulizi lililoanzishwa na Dowman kabla Gabriel Martinelli hajamtengea mpira Gabriel Jesus ambaye shuti lake liligonga Nathaniel Clyne na kujaa wavuni. Noni Madueke aliongeza bao la pili mapema kipindi cha pili kupitia mpira wa kona uliosisitiza ubora wa Arsenal katika mipira hiyo msimu huu.

Crystal Palace walipata bao lao dakika za mwisho kupitia Jean-Philippe Mateta, huku bao jingine la Yéremy Pino likikataliwa kwa kuotea. Hata hivyo matokeo hayo hayakubadili chochote kuhusu hatima ya ubingwa ambao tayari ulikuwa umeamuliwa.

Arsenal walimaliza msimu wakiwa na ushindi 26 na tofauti ya pointi saba juu ya wapinzani wao wa karibu. Aidha, wameweka rekodi mpya kwa kuwa timu ya kwanza katika historia ya Premier League kumaliza msimu mzima bila kuruhusu penalti wala kupata kadi nyekundu.

Kwa Arteta na mashabiki wa Arsenal, ubingwa huo unaashiria mwisho wa kipindi kirefu cha maumivu na mwanzo wa enzi mpya ya mafanikio. Baada ya miaka mingi ya kusubiri, Arsenal sasa wanarejea rasmi katika hadhi yao ya kuwa mabingwa wa England.

Join Our Newsletter!

Get updates, news etc from us. Its simple just put in your email address.

You may also read!

Safari ya Messi na Lamine Yamal Iliyotikisa Historia ya Soka

Soka lina uwezo wa kuandika simulizi ambazo hata waandishi wa riwaya hawawezi kuzibuni. Fainali ya Kombe la Dunia kati

Read More...

Serikali ya Marekani yaichangia Tanzania bilioni 2.63

Serikali ya Marekani imetoa zaidi ya Dola za Marekani milioni moja, sawa na takribani Sh. biliooni 2.63 ili kusaidia

Read More...

Tanzania, Marekani zasaini makubaliano ya Dola Bilioni 3.14 kuimarisha sekta ya afya

Serikali za Tanzania na Serikali ya Marekani zimesaini Hati ya Makubaliano (MoU) ya ushirikiano katika sekta ya afya ya

Read More...

Leave a reply:

Your email address will not be published.

Mobile Sliding Menu