Shirikisho la Soka barani Afrika, Confederation of African Football (CAF), limeitunuku Morocco ubingwa wa mashindano hayo kufuatia uamuzi wa bodi ya rufaa uliotolewa siku 58 baada ya mchezo wa fainali uliochezwa Januari 18 mjini Rabat, Morocco.
Awali, Senegal ilikuwa imetangazwa mshindi wa fainali hiyo baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Morocco katika mchezo uliokuwa na ushindani mkali. Hata hivyo, mechi hiyo iligubikwa na utata mkubwa baada ya wachezaji wa Senegal kususia kuendelea na mchezo wakipinga maamuzi ya mwamuzi, hususan kutolewa kwa mkwaju wa penalti katika dakika za mwisho wakati matokeo yakiwa 0-0.
Mchezo huo ulisimama kwa takribani dakika 17 huku hali ya taharuki ikitawala uwanjani. Baadaye, wachezaji wa Senegal walirejea uwanjani kuendelea na mchezo kufuatia juhudi za kuwashawishi zilizofanywa na mshambuliaji nyota Sadio Mané. Penalti ya Morocco iliyopigwa na Brahim Díaz iliokolewa na kipa Edouard Mendy kabla ya Senegal kufunga bao la ushindi kupitia Pape Gueye katika muda wa nyongeza.
Hata hivyo, baada ya mchezo huo, Morocco iliwasilisha rufaa kwa CAF ikipinga matukio yaliyojitokeza wakati wa mchezo. Katika uamuzi wake uliotolewa na bodi ya rufaa, CAF imebainisha kuwa Senegal ilikiuka kanuni za mashindano, na hivyo “inachukuliwa kuwa imepoteza mchezo huo kwa kufungwa mabao 3-0.”
Kutokana na uamuzi huo, Morocco imepewa ushindi rasmi wa mechi hiyo pamoja na ubingwa wa mashindano hayo. Aidha, CAF imetangaza adhabu mbalimbali, zikiwemo faini kwa pande zote mbili, huku baadhi ya hoja za rufaa za Morocco zikikubaliwa na nyingine kukataliwa.
Uamuzi huo umeibua mjadala mpana katika duru za soka, na unaingia katika historia kama mojawapo ya maamuzi yenye utata mkubwa kuwahi kufanywa katika soka la Afrika.



