Jimbo Kuu la Kanisa Katoliki la Dar es Salaam limetangaza kwa masikitiko makubwa kifo cha Mwadhama Polycarp Cardinal Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo hilo. Kwa mujibu wa taarifa rasmi, Kardinali Pengo amefariki usiku wa kuamkia leo majira ya saa 4:00 akiwa amelazwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), jijini Dar es Salaam, alipokuwa akipatiwa matibabu. Taarifa hiyo imetolewa na Askofu Mkuu wa Dar es Salaam, Thaddeus S. Ruwa’ichi, ambaye ameeleza kuwa ratiba na taratibu za mazishi zitatangazwa baadaye mara baada ya mipango kukamilika. Jimbo Kuu limewaomba waumini na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kuliombea Kanisa na kumuombea marehemu apate pumziko la milele.



