Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inajiandaa kumwapisha Felix Tshisekedi kuwa rais mpya wa taifa hilo mnamo wiki hii. Sherehe za kuapishwa zinatarajiwa kufanyika Alhamis wiki hii, na zitashuhudia Tshisekedi akiapishwa kuwa rais akichukua mikoba ya Joseph Kabila, aliyeitawala Congo tangu mwaka 2001. Awali sherehe hizo zilikuwa zifanyike leo Jumanne, lakini msemaji wa muungano wa upinzani CACH ambao ulimuunga mkono Tshisekedi, alisema uwezekano wa kuapishwa ni Alhamisi. Mahakama ya katiba ilitupilia mbali madai ya mgombea aliyeshika nafasi ya pili Martin Fayulu na kumthibitisha Tshisekedi kuwa rais mteule wa Congo. Mataifa kadhaa ya Afrika ikiwa ni pamoja na Jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika SADC na Kenya zimempongeza Tshisekedi. Burundi na Tanzania, ambazo zinashirikiana na Congo kwenye mapambano dhidi ya waasi, pia zimetuma pongezi.



