Zanzibar, Juni 17, 2026 – Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, anatarajiwa kuondoka Zanzibar leo kuelekea Mombasa, Kenya, kwa ziara ya kikazi ya siku mbili ambapo atamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano wa 11 wa Masuala ya Bahari (11th Our Ocean Conference).
Safari hiyo itaanza kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, huku mkutano huo wa kimataifa ukiendelea Mombasa kuanzia Juni 16 hadi 18, 2026, chini ya kaulimbiu ya “Our Ocean, Our Heritage, Our Future.”
Mkutano huo, ambao kwa mara ya kwanza unafanyika katika Bara la Afrika, unawakutanisha viongozi wa serikali, mashirika ya kimataifa, sekta binafsi, wataalamu, watafiti, asasi za kiraia pamoja na vijana kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika kulinda bahari na kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali zake.
Mijadala ya mkutano huo inalenga masuala muhimu yanayohusu hifadhi za bahari, uvuvi endelevu, mapambano dhidi ya uchafuzi wa mazingira ya baharini, maendeleo ya Uchumi wa Buluu, kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuimarisha usalama wa bahari.
Akiwa nchini Kenya, Dkt. Mwinyi anatarajiwa kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP), Bi. Inger Andersen, pamoja na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Shirikisho la Somalia, Hamza Abdi Barre, kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu mazingira, uchumi wa buluu na ushirikiano wa kikanda.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi atashiriki katika hafla ya kufunga Mkutano wa 11 wa Masuala ya Bahari tarehe 18 Juni 2026, hatua inayodhihirisha dhamira ya Tanzania katika kuendeleza Uchumi wa Buluu na matumizi endelevu ya rasilimali za bahari kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Baada ya kukamilisha ziara hiyo ya kikazi, Dkt. Mwinyi anatarajiwa kurejea Zanzibar tarehe 19 Juni 2026.



