JUMLA YA WATU 2249 VISIWA VYA MULEBA WAPATIWA ELIMU YA UGONJWA WA MARBURG .

In Afya, Kitaifa

Baadhi ya Watalaam wa Afya kutoka Wizara ya Afya wakitoa Elimu katika kisiwa Cha Rushonga kilichopo ndani ya ziwa Victoria Wilayani Muleba Mkoani Kagera  jinsi ya kumhudumia mgonjwa wa Marburg  Kwa kuchukua tahadhari.

Baadhi ya wananchi katika kisiwa Cha Nyaburo ndani ya ziwa Victoria Wilayani Muleba Mkoani Kagera wakifuatilia Elimu namna ya kujikinga na Marburg na tahadhari mbalimbali zinazotakiwa kuchukuliwa.


Mtaalam wa ufuatiliaji wa Magonjwa kutoka Wizara ya Afya  Emmanuel Mwakapasa akitoa maelekezo kwa watumishi kada ya Afya namna ya utoaji elimu juu ya ugonjwa wa Marburg ndani ya meli ya matibabu katika kisiwa cha Rushonga ziwa Victoria Wilaya ya Muleba Mkoani Kagera.

Daktari Kiongozi wa meli ya matibabu Mv Jubilee Hope iliyo chini ya Kanisa la AICT Dayosisi ya Geita.

Mtalaam wa Afya kutoka mkoni Kagera Rashid  Salum akifanya Huduma ya Utakasaji ili kuondoa vimelea vya Magonjwa katika makazi ya watu.


Sehemu ya mwalo wa kisiwa cha Kerebe ziwa Victoria Wilayani Muleba Mkoani Kagera ambapo huduma mbalimbali za kijamii hufanyika hivyo elimu juu ya ugonjwa wa Marburg ilitolewa katika maeneo haya.

Meli ya MV Jubilee Hope inayotumika katika utoaji WA huduma za afya katika visiwa vya Muleba Mkoani Kagera.

Na.Elimu ya Afya kwa Umma.

Katika jitihada za Wizara ya Afya ,Idara ya Kinga, Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma ya  kuhakikisha elimu ya kujikinga na ugonjwa wa Marburg  inamfikia kila mtanzania tangu utolewe taarifa hapa nchini, takriban jumla ya watu 2249  wamefikiwa na Elimu hiyo   katika visiwa vya Goziba, Kerebe, Makibwa, Rushonga  na Nyaburo vilivyopo ndani ya Ziwa Victoria Wilayani Muleba Mkoani Kagera.

Akizungumza mara baada ya timu ya Watalaam wa afya 14  kutoka Wizara ya Afya  kuhitimisha ziara ya uelimishaji  katika visiwa hivyo kwa ushirikiano nan a wadau mbalimbali ikiwemo  Usafiri wa meli  ya matibabu ya  MV Jubilee Hope chini ya Kanisa la AIC Tanzania Dayosisi ya  Geita, Mtalaam wa Ufuatiliaji wa Magonjwa kutoka Wizara ya Afya, Emmanuel Mwakapasa amesema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imefanikiwa kufikia makundi mbalimbali ya watu ikiwemo  wavuvi  1300,wananchi  900 pamoja na wahudumu wa afya  ngazi jamii 28 na Wahudumu wa Afya Vituoni 21.

“Kuna timu ya Wataalam 14  kutoka Wizara ya Afya walitumwa kwenye visiwa vilivyopo ziwa Victoria kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba kwa ajili ya utoaji wa elimu namna ya kuchukua hatua za kinga katika kukabiliana na Ugonjwa wa Marburg  ikiwemo kunawa mikono kwa maji safi tiririka na sabuni ya maji  na uelewa jinsi unavyonezwa “amesema.

Mwakapasa ameweka mchanganuo wa visiwa vilivyofikiwa ni pamoja na Goziba ambapo wavuvi 600 walipatiwa elimu ,wananchi 400 pamoja na wahudumu wa afya kituoni 7 na Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii 7; visiwa vya Kerebe na Makibwa wavuvi 300 , wananchi 200, na wahudumu wa afya kituoni 6, Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii 9; huku visiwa vya Rushonga na Nyaburo wakiwa wamefikiwa wavuvi 400,wananchi 300 na wahudumu wa afya kituoni 8 na Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii 12 ikiwa ni jumla  ya watu 2249 wakifikiwa na huduma hiyo ya  elimu  juu ya Ugonjwa wa Marburg.

Aidha, Mwakapasa ametaja dalili za Ugonjwa wa Marburg kuwa ni pamoja na homa kali , uchovu wa mwili,  kuumwa kwa misuli, maumivu ya tumbo, kuharisha, kuharisha damu, kutapika damu, ,macho kuwa mekundu , kutoka damu matundu mbalimbali ya mwili ikiwemo machoni, masikioni, puani, mdomoni na sehemu zingine za haja kubwa na haja ndogo hivyo kila mtu aonapo dalili kama hizo ni vyema kutoa taarifa kwa mtalaam wa afya mara moja.

Naye Daktari kiongozi wa meli ya matibabu Jubilee Hope Dkt. Uzia Mohammed amesema huduma ya matibabu tembezi ndani ya ziwa Viktoria katika visiwa vilivyopo Muleba walianza tangu mwaka 2015 huku akiishukuru serikali kwa kuwa na ushirikiana katika kukabiliana na Marburg kwa utoaji wa elimu.

“Ninaishukuru sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  kupitia Wizara ya Afya kwa kutuma timu ya watalaam kuelimisha visiwa vya Muleba katika kuhakikisha ugonjwa huu hausambai na sisi tumekuwa bega kwa bega “amesema.

Diwani kaya ya Goziba Mataba Mataba ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa maamuzi ya kufanya hatua wananchi wa visiwa hivyo vinafikiwa na watalaam wa afya kwani eneo hilo halifikiki kiurahisi.

“Namshkuru sana Rais  Dkt.Samia Suluhu Hassan pamoja na Wizara ya Afya kwa kuwakumbuka wananchi wa Goziba katika janga hili la Marburg hivyo kupitia mafunzo haya kuanzia sasa tumekuwa na mwitikio katika kuzingatia kanuni za afya “amesema.

Mganga Mfawidhi Zahanati ya Goziba Alhaji Ally amesema mafunzo hayo yatasaidia katika ufuatiaji wa Magonjwa  hivyo imeaongezea msukumo wa utoaji wa elimu kwa kushirikiana na Wahudumu wa Afya ngazi ya jamii .

“Tumetenga vyumba maalum kwa ajili ya kuwahifadhi wahisiwa kwa muda katika kisiwa hiki hivyo kupitia mafunzo haya ambayo yametolewa na wataalam wa afya yatatusaidia kujua zaidi namna ya ufuatiliaji wa magonjwa “amesema.

Licha ya Elimu ya afya juu ya ugonjwa wa Marburg kutolewa katika visiwa hivyo, huduma mbalimbali pia zilitolewa ikiwemo usafi wa mazingira, pamoja na huduma mbalimbali za matibabu.

Ikumbukwe kuwa   hivi karibuni Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu alisema  uchunguzi wa Maabara ya Taifa ulithibitisha uwepo wa virusi vya Marburg ambavyo vinasababisha ugonjwa wa Marburg Virus Disease (MVD) katika  Mkoa wa Kagera ambao umesababisha vifo vya Watu watano hadi sasa ambapo  Ugonjwa huo hauna tiba mahususi bali hutibiwa kwa dalili anazokuwa nazo Mgonjwa.

Hata hivyo, Waziri Ummy alisema kwa sasa hali salama  na hakuna maambukizi mapya na kuwataka wananchi hasa Kijiji cha Ntoma   Kagera na Watanzania kwa Ujumla  kuondoa hofu na kuendelea kuchukua tahadhari ambapo hadi sasa watalaam wa afya kutoka wizarani kwa kushirikiana na mkoa wamepiga kambi mkoani Kagera  kwa ajili ya utoaji elimu katika kuhakikisha maambukizi ya Marburg yasiendelee kusambaa  

Kwa mujibu wa taarifa za Shirika la Afya Duniani (WHO), ugonjwa huu wa Marburg uligundulika kwa mara ya kwanza Ujerumani mwaka 1967 katika Mji wa Marburg na ndio asili ya jina la ugonjwa huu na ulishawahi kutolewa taarifa katika nchi mbalimbali za Afrika na Ulaya .

Join Our Newsletter!

Get updates, news etc from us. Its simple just put in your email address.

You may also read!

WAZIRI MKUU MAJALIWA AKAGUA BARABARA YA SOMANGA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa asubuhi ya leo  Aprili 16, 2025 amewasili eneo la Somanga kukagua Miundombinu ya barabara kuu

Read More...

HATUTAWAACHIA CCM NAFASI TUTASHIRIKI UCHAGUZI MKUU – ACT WAZALENDO

Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Dorothy Semu amesema chama hicho kitashiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka

Read More...

Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Gissima Nyamohanga Afariki Dunia 

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Mhandisi Gissima Nyamohanga amefariki dunia usiku wa kuamkia leo katika ajali

Read More...

Leave a reply:

Your email address will not be published.

Mobile Sliding Menu