
Aliyekuwa Rais wa Marekani wa 41, George H W Bush amelazwa hospitalini kwa sababu ya kusumbuliwa na maradhi ya bakteria siku moja baada ya kuhudhuria mazishi ya mkewe Barbara.
Vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti kuwa Bush amelazwa katika kitengo cha uangalizi wa karibu. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na msemaji wa familia, kiongozi huyo aliyeiongoza Marekani tangu mwaka 1989 hadi 1993 amepatwa na maambukizi yaliyoenea kwenye damu, lakini “matibabu yake yanaendelea vizuri”.
Bush mwenye miaka 93 alipokelewa katika Hospitali ya Houston, siku ya Jumapili asubuhi.



