Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amemuagiza Kaimu Mhandisi wa
Wilaya ya Kondoa, Felcitism Tesha kung’oa milango yote katika Kituo cha Afya Busi kutokana
kutokuwa na viwango vya kuridhisha.
Ametoa agizo hilo alipofanya ziara ya kikazi katika Kijiji cha Busi wilayani Kondoa kukagua
utekelezaji wa miradi ya Ujenzi wa Vituo vya Afya vinavyojengwa kwa fedha za Serikali.
Dkt. Kijaji ambaye pia ni Mbunge wa Kondoa Vijijini amesema hajaridhishwa na milango
iliyowekwa katika kituo hicho kwa kuwa ubora wake hauendani na thamani ya fedha
iliyotolewa kwa ajili ya utengenezaji wa milango hiyo.
Alisema fedha iliyotengwa kwa ajili ya milango hiyo ni kubwa zaidi ya milango inavyoonekana,
hali inayo sababisha kuhatarisha usalama wa wagonjwa na watumishi wa kituo hicho.
“Nina agiza milango yote iliyowekwa ikiwa chini ya kiwango ibadilishwe kwa
gharama za fundi aliyepewa tenda hiyo bila kutumia hata shilingi moja ya
Serikali, milango haina hata mwaka imeanza kupasuka.”,alisisitiza Dkt. Kijaji.
Aidha, alitoa wito kwa Uongozi wa Wilaya kwa kushirikiana na Kamati ya Ujenzi ya Kijiji hicho
kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kikamilifu katika kusimamia miradi mbalimbali ya
maendeleo inayofadhiliwa na Serikali ili kubaini mapungufu na kuyafanyia kazi mapema.



