KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, GERSON MSIGWA, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. SAMIA SULUHU HASSAN imeendelea kujenga uchumi wa kujitegemea, amesema kiwango cha kujitegemea kwa uchumi kimeongezeka kutoka chini ya asilimia 50 miaka michache iliyopita hadi kufikia asilimia 74.2 kwa sasa.
MSIGWA, amesema hayo Jijini wakati akizungumza na waandishi ambapo amesema kuwà mafanikio hayo ni uthibitisho wa utekelezaji mzuri wa sera na mipango ya Serikali inayolenga kuimarisha uchumi wa Taifa na kuongeza uwezo wa nchi kujitegemea katika kugharamia maendeleo yake
Amesema kuwà, hivyo inaonyesha uimara wa uchumi wa Taifa na matokeo ya juhudi za Serikali katika kuimarisha uzalishaji, kuvutia uwekezaji na kusimamia sera za uchumi zinazolenga ustawi wa wananchi na maendeleo endelevu ya nchi.
Ameongeza kusema kuwà , ziara za kimkakati zilizofanywa na Rais Dkt. SAMIA SULUHU HASSAN nchini Urusi, Singapore na mwenyeji wake wa Rais wa Namibia zimeimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kidiplomasia, huku akitangaza kuwa Rais wa Msumbiji DANIEL CHAPO atafanya ziara ya kikazi nchini Julai 2 hadi 3, 2026 na kushiriki ufunguzi wa Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).
MSIGWA ,amesema uchumi wa Tanzania umeendelea kuimarika ambapo ukuaji wa uchumi ulifikia asilimia 5.9 mwaka 2025 na unatarajiwa kufikia asilimia 6.3 mwaka 2026.
Pia amesema Serikali inaendelea kutumia mikopo kugharamia miradi ya maendeleo yenye tija ikiwemo miradi mikubwa ya umeme, barabara na miundombinu mingine, amesema deni la Taifa bado ni himilivu kwa mujibu wa viwango vya kimataifa.
Amesema kukamilika kwa Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere kumeongeza uzalishaji wa umeme na kuimarisha upatikanaji wa nishati nchini.
Pia amewahakikishia Watanzania kuwa Serikali itaendelea kulinda amani na kuhakikisha huduma za kijamii pamoja na miradi ya maendeleo vinaendelea kutekelezwa kwa ufanisi.



