Jeshi la Korea Kusini limesema Korea Kaskazini imerusha makombora kadhaa ya masafa mafupi kutoka pwani yake ya mashariki leo hii. Korea Kusini imesema makombora hayo yalirushwa kutoka mji wa Wonsan wa Korea Kaskazini milango ya saa tatu asubuhi leo saa za Korea. Korea Kusini imeeleza kwamba inafanya uchunguzi kuhusu makombora hayo, ikishirikiana na Marekani. Ni makombora ya kwanza kurushwa na Korea Kaskazini tangu mwezi Novemba 2017. Harry Kazianis wa gazeti la Marekani masuala ya kimataifa la The National Interest, amesema hatua hiyo inaonyesha wazi kwamba Korea Kaskazini imekasirishwa na msimamo wa Marekani wa kuishinikiza nchi hiyo kusimamisha mpango wake wa kinyuklia lakini bila ya kuikubalia kuiondolea vikwazi ilivyoiwekea. Viongozi wa nchi hizo mbili Kim Jong-Un na Donald Trump wameshakutana mara mbili katika mikutano ya kilele lakini wameshindwa kufikia makubaliano.



