Mama wa msanii wa muziki wa Hip-hop nchini, Rashid Abdallah maarufu kama Chid Benz, Hawa Idd Mwamanda, amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Februari 11, 2025, nyumbani kwake.

Akithibitisha taarifa za msiba huo, Chid Benz amesema kuwa kwa sasa msiba upo nyumbani kwao mtaa wa Masantula, Chanika jijini Dar es Salaam. Ameeleza kuwa wakati taarifa za kifo hicho zinamfikia alikuwa studio na anaelekea nyumbani kushiriki katika taratibu za awali za msiba.
Msanii huyo amesema amekuwa akipokea maswali mengi kuhusu mipango ya mazishi, lakini amesisitiza kuwa uamuzi rasmi utatolewa na kaka yake mkubwa baada ya familia kukamilisha mashauriano. Ameongeza kuwa ni vyema watu wakafika nyumbani kwa marehemu ili, endapo mazishi yatafanyika leo, waweze kushiriki pamoja na familia.
Taarifa rasmi kuhusu ratiba na taratibu za mazishi zinatarajiwa kutolewa baadaye na familia.



