MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesema kwamba licha ya kufungia mamia ya vituo vya mafuta nchi nzima, leo itaendelea na operesheni hiyo ya kufunga vituo vingine vya mafuta ambavyo havijafunga moja kwa moja mashine za malipo za kielektroniki (EFDs) na pampu.
Kamishna wa Kodi za Ndani wa TRA, Elijah Mwandumbya amesema jana kuwa watu ambao TRA imewafungia vituo vyao, watafunguliwa tu iwapo watakidhi vigezo ambavyo ni pamoja na kulipia mashine na kuingia makubaliano na mamlaka hiyo, kuwa ni muda gani mafundi watakuwa wamefunga mashine hizo.
Mwandumbya amesema kwa sasa TRA haitaruhusu wenye vituo vya mafuta waendelee kutumia mashine za mkono ambazo ziko nje ya mashine kwani wametumia mwanya huo kukwepa kodi ya serikali.
Amesema kati ya watu 10 wanaojaza mafuta, ni wawili tu ndio walikuwa wanapewa risiti hizo tena kwa kuzidai.
