Mazulia ni mapambo mazuri na yenye kupendezesha nyumba hasa yakiwekwa kwenye mpangilio wa kuvutia. Yapo mazulia ya aina mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya maeneo tofauti mfano sebuleni, dining room, mlangoni, bafuni, chumbani n.k. Hapa nitaongelea mazulia ya saizi ya kati na madogo.
Tukianza na mazulia ya sebuleni na dining room, kwanza kabisa yasiwe makubwa sana hadi kuziba sakafu yote, yawe ya saizi ya kati ya kufunika eneo la chiniya meza na chini ya makochi / viti miguu ya mbele iwe kwenye zulia na ya nyuma kwenye sakafu ya kawaida. La muhimu kuzingatia ni kuwa rangi ya zulia isiachane sana na rangi ya sakafu / tiles, rangi ya makochi na pia rangi ya mapazia. Sio kusema viwe na rangi moja, hapana bali viwe na rangi zinazoendana ili kuleta uwiano na mvuto na sio kuumiza macho au kufanya sebule / dining room kuonekana ipo ovyo ovyo.
Mazulia ya mlango wa nje yawe magumu kidogo zaidi ya yale ya milango ya ndani na yawe na upana sawa na mlango. Bafuni yanafaa yawe ya plastiki maana maji ni mengi na zulia la nyuzi litalowana kwa urahisi na kutoa harufu au kuharibika. Yale ya chumbani yanapendeza zaidi yakiwa na nyuzi nyingi na laini ili kukupa mguso mzuri unapoamka asubuhi au unapojiandaa kulala.
