Mfalme wa Japan Akihito ametangaza kuachia wadhifa wake katika hotuba yake ya mwisho kwa watu wake. Kwenye sherehe iliyofanyika katika kasri lake leo Akihito mwenye umri wa miaka 85 pia aliwapongeza watu wa Japan kwa kumuunga mkono wakati wa uongozi wake wa miaka 30 akiwa Mfalme. Utawala wa Akihito unakamilika rasmi saa sita za usiku saa ya Japan, ambapo mwanawe wa kiume Naruhito atachukua wadhifa wa kuwa mfalme mpya. Sherehe ya kuapishwa Naruhito itafanywa kesho. Tukio la Akihito kuachia ufalme ni la kwanza kwa mfalme wa Japan katika karibu miaka 200 iliyopita. Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe ni miongoni mwa wageni wanaohudhuria hafla hiyo. Viongozi mbalimbali duniani wanaendelea kutuma salamu za pongezi kwa Mfalme huyo anayeondoka. Rais wa Korea Kusini Moon Jae-in na mwenzake wa Marekani Donald Trump wametoa shukrani kutokana na mchango wake wa kuhimiza ushirikiano na amani baina ya mataifa yao.