Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina amezindua mafunzo rejea kwa maafisa Ugani na Wafugaji wilayani Simanjiro mkoani Manyara, kwa kuwataka wafugaji na maofisa hao kuhakikisha kuwa wanayatumia vyema ili kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya Mifugo nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Mpina amesema kuwa wizara ya mifugo na uvuvi inaendesha mafunzo hayo kwa mara ya kwanza na kwa nchi nzima lengo likiwa ni kuamsha Ari kwa ugani na kuongeza uwajibikaji ambapo yatazinduliwa tena wilayani kaliuwa mkoani Tabora.
Mpina amesema kuwa maofisa Ugani wanapaswa kukumbushwa mahusiano yao na wafugaji lakini pia kutambua sheria mbali mbali ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima.
Aidha amesema mafunzo mengine yatalenga kuwajengea uwezo wafugaji kutambua nafasi zao za namna ya kuweka Akiba,Kupata nyumba bora,uhifadhi salama wa fedha na kupata mbegu bora za mifugo pamoja na malisho.
Kwa Upande wake Mkurugenzi wa utafiti ,mafunzo na ugani kutoka wizara ya mifugo na Uvuvi daktari Angello Mwilawa amewataka wananchi kote nchini,kuhudhuria mafunzo hayo kikamilifu.



