Mwanajeshi mmoja wa kikosi cha Jumuia ya Kujihami ya NATO, kutoka Jamhuri ya Czech ameuawa katika shambulizi lililotokea kwenye jimbo la Herat, Afghanistan na wengine wawili wamejeruhiwa.
Taarifa iliyotolewa na kikosi cha NATO mjini Kabul, imeeleza kuwa shambulizi hilo limefanywa na askari wa vikosi vya usalama vya Afghanistan.
Maafisa wa jeshi la Jamhuri ya Czech wamesema kuwa wanajeshi waliojeruhiwa walikimbizwa katika hospitali ya kijeshi ya Bagram.
Mwanajeshi mwingine wa NATO aliuawa mashariki mwa Afghanistan mwanzoni mwa mwezi huu wa Oktoba.
Mwezi Agosti, wanajeshi watatu wa NATO kutoka Jamhuri ya Czech waliuawa katika shambulizi la kujitoa muhanga pia mashariki mwa Afghanistan.
Kikosi cha NATO kinatoa ushauri na kuwapatia mafunzo wanajeshi na wafanyakazi wa vikosi vya usalama vya Afghanistan.
Jamhuri ya Czech ina kiasi ya wafanyakazi 350 wa kijeshi nchini Afghanistan.



