Duru mpya ya mazungumzo ya kutafuta amani Syria ilianza jana mjini Geneva huku serikali ya Syria ikanusha vikali madai kuwa iliwachoma maelfu ya wafungwa kwa tanuri katika gereza moja ili kuficha ushahidi wa mauaji ya maelfu ya wafungwa.
Duru tano zilizopita za mazungumzo ya kujaribu kuvimaliza vita vya Syria ambavyo vimedumu kwa zaidi ya miaka sita hazijaweza kufanikiwa kuutatua mzozo huo.
Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria Steffan Di Mistura alikutana jana na ujumbe wa serikali ya Syria na wa upinzani katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa.
Matumaini ya kuumaliza mzozo wa Syria ni madogo huku madai hayo kuwa maelfu ya wafungwa wanauawa na kisha kuchomwa katika gereza la Saydnaya yakizidisha uhasama kati ya pande mbili zinazozana.
Mazungumzo hayo yanatarajiwa kukamilika mwishoni mwa wiki hii.
Vita vya Syria vimesababisha vifo vya zaidi ya watu laki tatu
