Maelfu ya watu wanaotoroka mapigano makali yanayoendelea katika Jamhuri ya Afrika ya Kati wanamiminika katika nchi jirani ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo baada ya ghasia zinazochewa na uhasama wa kidini kuzuka katika mji wa mpakani wa Bangassou.
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwashughulikia wakimbizi UNHCR limesema mmiminiko huo wakimbizi ni mkubwa na takriban watu 2,750 waliwasili kaskazini mwa Congo mwishoni mwa wiki iliyopita na wengine wengi bado wanawasili.
Wanajeshi sita wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa waliuawa katika mji huo wa Bangassou katika shambulizi lililofanywa na waasi wa kundi la Anti Balaka. Zaidi ya raia 100 pia waliuawa katika ghasia hizo kati ya makundi ya waasi ya Kikiristo na Kiislamu.
UNHCR imesema Congo ambayo yenyewe inakumbwa na ghasia tangu mwishoni mwa mwezi Machi, inawahifadhi wakimbizi zaidi ya laki moja kutoka Jamhuri ya Afrika ya kati.
