Tanzania yagundua Dawa ya Tezi Dume, Iko kwenye hatua za mwisho

In Afya
TANZANIA iko kwenye hatua za kuridhisha katika utafiti wa miti maalumu inayoaminika itakuwa chanzo cha dawa maalumu ya kuzuia na kutibu maradhi sugu ya tezi dume pamoja na saratani ya kibofu, matatizo yanayowasibu wanaume wengi duniani.
Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela iliyopo eneo la Tengeru wilayani Meru mkoani Arusha, inafanyia utafiti mti mwekundu wa asili ujulikanao kama ‘kiburabura,’ unaopatikana katika msitu wa Magamba wilayani Lushoto mkoani Tanga.
Ingawa katika hali ya kawaida utomvu wa mti huo wa kiburabura (unaojulikana kisayansi kama Prunus Africana) unadaiwa kuwa ni sumu, lakini wanasayansi kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela wanasema hilo hasa ndilo litakuwa chimbuko la tiba ya uhakika kwa matatizo ya tezi dume, saratani ya kibofu na magonjwa mengine ya viungo vya uzazi.
Makamu Mkuu wa Taasisi ya Nelson Mandela, Dk Mussa Chacha alisema mjini hapa kuwa, utafiti huo wa miti hiyo ya asili kwa ajili ya tiba, ulianza miezi sita iliyopita na kwamba upo katika hatua nzuri, ingawa hakusema kuwa watakamilisha lini mradi huo ili kuifanya Tanzania kuingia kwenye historia ya dunia kama wavumbuzi wa tiba ya maradhi hayo yanayowasumbua wanaume wengi duniani na hata kusababisha vifo.
Alikuwa akitoa maelezo ya chuo hicho cha Nelson Mandela kwa Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako aliyekuwa anazitembelea taasisi kadhaa za sayansi na teknolojia mkoani hapa, kikiwemo Chuo cha Nelson Mandela (NM-AIST) na Tume ya Mionzi (TAEC).
“Kutokana na uharibifu wa mazingira na miti kukatwa hovyo, hivi sasa mti huu wa kiburabura umeanza kutoweka nchini, lakini kuna baadhi ya mimea hii ambayo inapatikana katika msitu wa Magamba wilayani Lushoto na tayari wenyeji wa eneo hilo wanakiri kutumia magamba ya mti huo kwa ajili ya tiba za malaria na matatizo ya viungo vya uzazi,” alisema mkufunzi huyo.
Zaidi ya wanaume 30,000 hufa kila mwaka kutokana na matatizo ya saratani ya kibofu. Ugonjwa huu mara nyingi huwapata watu wazima kuanzia umri wa miaka 45 na kuendelea.
Sasa wasomi wa Tanzania wako mbioni kugundua dawa ya moja kwa moja. Saratani ya tezi dume inashika nafasi ya tatu kwa kusababisha vifo kwa wanaume duniani.
Pia ni chanzo kikuu cha vifo kwa wanaume wenye umri wa miaka 70 na kuendelea.
Tafiti za Chama cha Saratani cha Marekani (ACS) na cha Afrika Kusini (CANSA) zimebaini kuwa, mwanamume mmoja kati ya sita hupata saratani ya tezi dume katika uhai wake.
Kutokana na takwimu za mwaka 2010 za dunia nzima, malaria iliua watu 500,000, kifua kikuu watu milioni 2.1, Ukimwi watu milioni 1.8 na saratani watu milioni 9.9.
Kwa mujibu wa takwimu hizo, idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na ugonjwa wa saratani ni kubwa ikilinganishwa na ya magonjwa mengine.
Dk Emmanuel Kandusi ambaye ni miongoni mwa waathirika wa saratani hiyo, na mwanzilishi wa kampeni ya kuangamiza saratani ya tezi dume Tanzania ya ‘50 Plus Campaign’ anasema ugonjwa huo ukitambuliwa mapema huweza kutibika kwa urahisi.
Ameongeza kuwa kutokana na ugonjwa huo kuwa hatari nchini humo, ifikapo mwaka 2020 unatarajiwa kuua watu milioni 20. Matibabu ya ugonjwa huo ni pamoja na kupata dawa pamoja na upasuaji.
Naye Profesa Ndalichako alisifu jitihada za Nelson Mandela katika kufanya tafiti zenye tija na kuongeza kuwa serikali imetenga zaidi ya Sh bilioni 8.3 kwa ajili ya maendeleo ya elimu katika taasisi hiyo ikiwemo vifaa vya maabara na utafiti pamoja na udahili wa wanafunzi.
Fedha hizo zikiwa ni mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Wakati huo huo, utafiti wa Taasisi ya Africa Capacity Building Foundation kwa mwaka huu unaonesha kuwa Tanzania iko katika nafasi ya pili barani Afrika katika matumizi ya sayansi na teknolojia kwa ajili ya kujiletea maendeleo

Join Our Newsletter!

Get updates, news etc from us. Its simple just put in your email address.

You may also read!

WANAFUNZI 500 WAPEWA MBINU WASILOWEE KWENYE MADAWA YA KULEVYA.

Na Tonie kaisoe ,Arusha Wanafunzi zaidi ya 500 wa shule ya Sekondari Arusha Jiji na Wilaya ya Arumeru wamepewa mbinu

Read More...

MR. IBU AFARIKI DUNIA

Mchekeshaji maarufu wa Nollywood nchini Nigeria, John Okafor, almaarufu Mr. Ibu amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Read More...

POLISI, LATRA WAPIGA FAINI MABASI YALIYO ZIDISHA NAULI ARUSHA.

Jeshi la Polisi kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha kwa kushirikaiana na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA)

Read More...

Leave a reply:

Your email address will not be published.

Mobile Sliding Menu