Rais wa Marekani Donald Trump ametia saini tangazo jipya linaloweka marufuku kali kwa raia wa mataifa 12 kuingia nchini humo, hatua ambayo inarejelea mkakati wake wa awali kuhusu udhibiti wa uhamiaji wa kimataifa. Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Marekani marufuku hiyo ilitangazwa Jumatano kwa kunukuu maafisa waandamizi wa utawala wa Trump.
Tangazo hilo linazuia raia kutoka nchi zifuatazo Afghanistan, Myanmar, Chad, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Guinea ya Ikweta, Eritrea, Haiti, Iran, Libya, Somalia, Sudan, na Yemen. Vyanzo vya habari vimeeleza kuwa hatua hiyo inalenga kuongeza usalama wa taifa na kudhibiti hatari za kigaidi na changamoto za kiusalama kutoka mataifa hayo.
Zaidi ya hapo, marufuku ya kiwango fulani pia imewekwa dhidi ya raia wa mataifa saba mengine ambayo ni Burundi, Cuba, Laos, Sierra Leone, Togo, Turkmenistan, na Venezuela. Hii inamaanisha kuwa baadhi ya aina za visa, kama za wahamiaji au zisizo za wahamiaji, zinaweza kusitishwa au kuwekewa masharti maalum.
Katika muhula wake wa kwanza, Rais Trump alishawahi kutangaza marufuku ya usafiri dhidi ya mataifa saba yenye idadi kubwa ya Waislamu, hatua iliyokumbwa na upinzani mkubwa wa kisheria. Hata hivyo, marufuku hiyo ilifutwa rasmi mwaka 2021 na Rais Joe Biden, aliyesema kuwa ilikuwa na athari mbaya kwa taswira ya Marekani duniani.



