Mkamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Mbarouk Salum Mbarouk ameviagiza vyama vya siasa nchini kuzingatia sheria za uchaguzi pamoja na
kanuni za uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.
Amesema endapo agizo hilo litazingatiwa, uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika baadaye mwaka huu na uchaguzi mkuu wa mwakani, utakuwa wa amani na
utulivu.
Akizungumza katika mkutano na wadau wa uchaguzi jana, Jaji Mbarouk alisema licha ya kuvitaka vyama vya siasa kuzingatia sheria za uchaguzi pia wadau wa uchaguzi
wanapaswa kutoa taarifa zilizo sahihi kwa wakati muafaka.
Amesema kila mwananchi mwenye sifa ya kuandikishwa kuwa mpiga kura anapaswa kujiandikisha na mwenye kuhitaji kuboresha taarifa zake atumie nafasi hiyo
kujitokeza ili kuboresha.
Alisema kwa upande wa Mkoa wa Mwanza, zoezi la uandikishwaji katika daftari la kudumu la wapiga kura litaanza Agosti 13, na litaendelea mpaka Agosti 19, mwaka huu.
Jaji Mbarouk amesema uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigaji kura safari hii halitahusisha wapiga kura wote walioandikishwa katika daftari la kudumu la mwaka
2015.
Alisema uboreshaji utawahusu wapiga kura wapya waliotimiza miaka 18 na wale watakaotimiza miaka 18 siku ya uchaguzi mkuu mwaka 2020.



