Watu karibu 22 wameuawa katika muda wa siku tatu za mapigano huko Jamhuri ya Afrika ya Kati. Wafugaji wenye silaha walikabiliana na wapiganaji wanamgambo katika mji wa kusini mashariki kuanzia siku ya Jumatano na milio ya risasi imeendelea kusikika hadi jana Ijumaa.
Ingawa chanzo cha mapigano hayo hakijajulikana, lakini wafugaji waliohusika katika mapigano hayo wanaaminika kuwa na mahusiano na kundi moja lililokuwa chini ya muungano wa kiislamu wa Seleka ambao umesambaratishwa.
Kundi hilo ndilo lililomuondoa rais Francois Bozize madarakani mwaka 2013.
Tangu wakati huo, maelfu ya watu wamepoteza maisha na wengine wengi wakiyakimbia makazi yao.
Umoja wa Mataifa umekadiria kuwa karibu watu 1000 wamekimbia makazi yao kutoka mkoa huo wa kusini mashariki baada ya machafuko ya wiki hii.
