Mwanamuziki mashuhuri wa mtindo wa Afrobeats nchini Uganda Ugandan Robert Kyagulanyi Ssentamu, maarufu kama Bobi Wine, ameshinda ubunge katika uchaguzi mdogo nchini humo.
Wine, ambaye aliwania kama mgombea huru, aliwashinda wagombea wengine wane katika eneo bunge la Kyadondo Mashariki katikati mwa Uganda.
Alipata kura elfu 25,659 kutoka kwa kura elfu 33,310 zilizopigwa, gazeti la serikali la New Vision limeripoti.
Gazeti hilo linasema baada ya kutangazwa mshindi, aliahidi kuangazia zaidi kuwaunganisha raia.
Mwanamuziki huyo alikuwa amekamatwa na polisi na kuhojiwa kwa muda kabla ya kuachiliwa siku chache zilizopita.
Kiti hicho cha ubunge kiliachwa wazi baada ya mahakama kuamua kuwa uchaguzi uliofanyika mapema mwaka jana haukufuata kanuni na sheria za uchaguzi.
Kiongozi wa chama cha upinzani cha FDC Kizza Besigye amempongeza mwanamuziki huyo kwenye Twitter.
