WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, kesho anatarajiwa kukabidhiwa taarifa za kamati mbili zilizoundwa na Bunge katika Mkutano wa Saba wa Bunge la 11 kuhusu na makinikia ya almasi na biashara ya madini ya tanzanite.
Kwa mujibu wa taarifa za bunge hafla fupi ya makabidhiano hayo itafanyika katika viwanja vya bunge na viongozi wa kitaifa watakuwepo.
Kabla ya Waziri Mkuu kukabidhiwa taarifa hizo, kamati hizo mbili zitakabidhi taarifa zake kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai ambaye naye atakabidhi kwa Waziri Mkuu.
Taarifa hizo mbili zinazosubiriwa kwa makini hasa baada ya taarifa za kamati zilizoundwa na Rais John Magufuli kuibua makubwa katika makinikia kwenye makontena bandarini.
Kamati hizo maalumu zote zilikuwa na idadi sawa ya wabunge ambao ni tisa na zililenga kushauri juu ya mfumo bora wa uchimbaji, usimamizi, umiliki na udhibiti wa biashara ya madini ya almasi na Tanzanite hapa nchini.
Aidha Kamati iliyohusu almasi ikiongozwa na Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu ilitajwa kabla ya kuhitimisha shughuli za Bunge la Bajeti.
Uundaji wa kamati hizo umefanyika kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli katika kukabiliana na ‘wizi’ wa mali asili za taifa.
