WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea kiwanda cha sukari cha TPC kilichopo Arusha Chini, wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro na kukagua baadhi ya miundombinu ya kiwanda pamoja na mashamba.
Akiwa kiwandani hapo, Waziri Mkuu ameelezwa kwamba hivi sasa msimu wa uzalishaji umefungwa, na kiwanda kinafanyiwa matengenezo ambapo alishuhudia baadhi ya mitambo ikiwa imefunguliwa na kufanyiwa ukarabati.
Akitoa taarifa juu ya matengenezo hayo, Meneja wa Kiwanda hicho, Bw. Pascal Petiot , amemweleza Waziri Mkuu kwamba kiwanda hicho kimefungwa kwa zaidi ya wiki sita ili kujiandaa na msimu ujao wa uzalishaji ambao uko karibuni kuanza.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa kiwanda hicho, Bw. Robert Baissac amesema uzalishaji wa sukari kwenye kiwanda hicho umepanda kwa asilimia zaidi ya 200, tangu wachukue kiwanda hicho mwaka 2000.
Amesema wakati wanaanza, kiwanda kilikuwa na uwezo wa kuzalisha tani elfu 36,000 kwa mwaka, na wakati wanakinunua walitakiwa kuongeza uzalishaji kwa asilimia 100, kwa kufikisha tani 72,000 za sukari.
Aidha Waziri Mkuu aliwataka wafanyakazi wa kiwanda hicho, wafanye kazi kwa bidii na kujituma na kuhakikisha wanaongeza tija katika uzalishaji wao.
