Waziri wa ulinzi wa Israel Avigdor Lieberman aliyejiuzulu jana akipinga kusitishwa kwa mapigano baina ya nchi yake na kundi la wapalestina la Hamas, ametaka ufanyike uchaguzi wa mapema, na kuiweka serikali ya waziri mkuu Banjamin Netanyahu katika hali tete. Lieberman mwenye msimamo mkali amekiondoa chama chake kutoka muungano unaoongozwa na Netanyahu, na kumuacha kiongozi huyo akiwa na wingi wa kiti kimoja tu bungeni. Netanyahu ameutetea mpango uliofikiwa Jumanne wa kusitisha mapigano na Hamas, ambayo yalikuwa makubwa zaidi tangu yale ya mwaka 2014. Netanyahu amechukuwa majukumu ya waziri wa Ulinzi, na chama chake cha Likud kimepuuza mwito wa Lieberman wa kuitishwa uchaguzi wa mapema. Chama kingine kilicho katika muungano wa serikali ya Netanyahu kinachoongozwa na mwanasiasa mwingine mwenye sera kali za kizalendo Naftali Bennett kimetishia pia kujitoa katika muungano huo, ikiwa hakitakabidhiwa wizara ya ulinzi.



