Jeshi la polisi wilaya na mkoa wa Lindi limefanikiwa kufyeka na kuteketeza shamba la bangi lenye ukubwa wa zaidi ya ekari mbili,na kukamata lita 177 za pombe haramu aina ya gongo na kuwashikilia jumla ya wanaume kumi na wanawake saba.
Ikiwa ni operesheni ya kawaida zinazofanywa na jeshi la polisi wilaya ya Lindi na ushirikiano wa raia wema, kikosi maalum kilifanya msako katika kijiji cha Mnali na kufanikiwa kukuta shamba lililosheheni miche ya bangi.
Jeshi la polisi likiongozwa na kamanda wa polisi wa mkoa wa Lindi,Kamishna msaidizi mwandamizi,Renatha Mzinga pamoja na kufuata taratibu za kisheria , waliteketeza shamba hilo.
Kwa mujibu wa sheria , Hakimu mkazi wa mahakama ya wilaya ya Lindi Erasto Yakobo Phili alishuhudia uwepo wa shamba hilo na kuamuru kuteketezwa.
